Na Agustino
Luambano.
Baadhi
ya wakazi wa kata ya Kunduchi Tegeta jijini Dar es salaam wameonesha wasiwasi
wao juu uwezekano wa eneo lililotumiwa kibiashara linalojulikana kama “Ugogoni”
kuendelea tena na shughuli zake zilizokuwa zinafanywa hapo awali licha ya jeshi la polisi kulizuia na
kubomoa eneo hilo.
Eneo
hilo lililokuwa likihusisha biashara ndogondogo kama vile; vinyozi, mama rishe,
pombe za kienyeji na pombe hatari ya gongo lilizuiwa na kuvunjwa na jeshi la
polisi baada ya wakazi wa eneo hilo kulalamika kuibiwa mali zao na vijana
waliokuwa wanashinda eneo hilo mchana kutwa wakisingizia kufanya biashara
katika eneo hilo.
Wakitoa
malalamiko yao kwa nyakati tofauti tofauti baadhi ya wakazi wa karibu na eneo
hilo ambao hawakutaka kutajwa majina yao walidai kuwa licha ya jeshi la polisi
kuwaondoa wafanyabiashara wa eneo hilo na kubomoa vibanda vyao kwa zaidi ya
miezi sita iliyopita, bado imeonekana kuwa kuna baadhi ya vijana ambao
wanaonekana kukaa katika vichaka vya eneo hilo ambalo kwa sasa ni kama msitu.
Fred
Msungu ambaye hakutaka kueleza cheo chake licha ya kuonekana kuwa na uongozi
katika eneo hilo alieleza kuwa “kilichowatoa watu hapa ni uuzaji wa gongo,
kuvuta bangi, ukahaba, na wizi. Hapa ilikuwa hakatizi mtu bila kuibiwa” Alisema
Fred.
Aidha
Bwana Fred aliongeza kuwa “baada ya
polisi kuwaondoa watu na kuvunja vibanda hapa, amani ilikuwepo na matukio ya
wizi yalitulia lakini sasa matukio hayo yameanza upya na bado tunawaona watu
wametulia pale Ugogoni wanafanya nini?” Alihoji Bwana
Fred Msungu.
Wakati
wa mchana walionekana vijana wachache wakiwa wamepumzika katika eneo hilo ambalo kwa
sasa ni eneo la wazi mali ya manispaa ya Kinondoni.Vijana hao ambao hawakutaka
kuhojiwa inadaiwa kuwa wakati wa usiku wanaongezeka na kufanya uhalifu.
No comments:
Post a Comment