NA SALOME MWASAMALE, DAR
KATIKA kukabiliana na changamoto ya soko
kwa wakulima wadogo wadogo benk ya Yetu microfinance kwa kushirikiana na
kampuni ya vijana ya kitanzania ya Green Terk na shirika la YOSEFO wameanzisha
mfumo wa kilimo cha pamoja (farm park) ili kuleta mapinduzi katika sekta ya
kilimo hapa nchini.
Akizungumza kwenye semina ya
wakulima wadogo kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini iliyofanyika jana jijini
Dar es salaam mkurugenzi mtendaji wa Yetu microfinance Bank Altemius Millinga
alisema mpaka sasa wakulima wadogo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa
masoko kutokana na kila mmoja kulima pekee yake.
“Dhana iliyopo hapa nchini ya
wakulima wadogo kila mmoja kulima pekee yake katika maeneo tofauti ndiyo
inayosababisha wakulima kushindwa kuzalisha kiasi cha kutosha hivyo kusababisha
ugumu wa upatikanaji wa soko” alisema Millinga.
Kufuatia hali hiyo alisema ndiyo
maana Yetu Microfinance Bank wameamua kuanzisha mfumo wa kilimo cha pamoja
(Farm Park) ili kuondokana na changamoto hiyo ambayo imekuwa sugu kwa wakulima
wadogo hapa nchini.
Katika mafunzo hayo wakulima hao
wamefundishwa namna ya kulima kilimo cha kisasa chenye tija cha Green House na kile
cha umwagiliaji kwa njia ya matone ili kupata mafanikio kutokana na kazi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki
wa semina hiyo mkulima Meinrad Lupenza alisisitiza kuwa wakulima wadogo wanania
ya dhati ya kujiletea maendeleo hivyo waliiomba Yetu Microfinance Bank
kuharakisha zoezi hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa Yetu Microfinance Bank Altemius Millinga akipanda mti kama ishara ya uzinduzi wa uanzishwaji wa kilimo cha pamoja (Farm park) picha na Salome Mwasamale.
No comments:
Post a Comment